23 Maana mimi nilipokea kwa Bwana yale maagizo niliyowaachieni: kwamba, usiku ule Bwana Yesu aliotolewa, alitwaa mkate,
24 akamshukuru Mungu, akaumega, akasema: "Huu ndio mwili wangu ulio kwa ajili yenu; fanyeni hivi kwa kunikumbuka."
25 Vivyo hivyo, baada ya kula, akatwaa kikombe akasema: "Hiki ni kikombe cha agano jipya linalothibitishwa kwa damu yangu. Fanyeni hivi, kila mnapokunywa, kwa kunikumbuka."
26 Maana kila mnapokula mkate huu na kunywa kikombe hiki, mwatangaza kifo cha Bwana, mpaka atakapokuja.
27 Kwa hiyo, kila aulaye mkate huo au kunywa kikombe cha Bwana bila kustahili, atakuwa na hatia dhidi ya mwili na damu ya Bwana.
28 Basi, kila mtu ajichunguze mwenyewe kwanza, ndipo ale mkate huo na anywe kikombe hicho;
29 maana anayekula na kunywa bila kutambua maana ya mwili wa Bwana, anakula na kunywa hukumu yake yeye mwenyewe.
30 Ndiyo maana wengi kati yenu ni dhaifu na wagonjwa, na wengine kadhaa wamekufa.