1 Habari hii ya yahusu Neno la uzima lililokuwako tangu mwanzo. Sisi tumepata kulisikia na kuliona kwa macho yetu wenyewe; tulilitazama na kulishika kwa mikono yetu wenyewe.

2 Uzima huo ulipotokea sisi tuliuona na sasa tunasema habari zake na kuwaambieni juu ya uzima huo wa milele uliokuwa kwa Baba na uliodhihirishwa kwetu.

3 Tulichokiona na kukisikia ndicho tunachowatangazieni ninyi pia ili nanyi mpate kushirikiana nasi katika umoja tulio nao na Baba na Mwanae Yesu Kristo.

4 Tunawaandikia ninyi mambo haya kusudi furaha yetu ikamilike.

5 Basi, habari tuliyoisikia kwake Yesu na tunayowahubirieni ndiyo hii: Mungu ni mwanga na hamna giza lolote ndani yake.

6 Tukisema kwamba tuna umoja naye,na papo hapo twaishi gizani, tutakuwa tumesema uongo kwa maneno na matendo.

7 Lakini tukiishi katika mwanga, kama naye alivyo katika mwanga, basi tutakuwa na umoja sisi kwa sisi, na damu yake Yesu Kristo, Mwanae, inatutakasa dhambi zote.

8 Tukisema kwamba hatuna dhambi, tunajidanganya wenyewe na ukweli haumo ndani yetu.

9 Lakini tukiziungama dhambi zetu, basi Mungu ni mwaminifu na mwadilifu, naye atatusamehe dhambi zetu na kututakasa na uovu wote.

10 Tukisema kwamba hatujatenda dhambi, tutakuwa tumemfanya Mungu mwongo, na neno lake halimo ndani yetu.