1 Hatimaye, ndugu zangu, mmejifunza kutoka kwetu namna mnavyopaswa kuishi ili kumpendeza Mungu. Na kweli mmekuwa mnaishi hivyo. Sasa tunawaombeni na kuwasihi kwa jina la Bwana Yesu mfanye vema zaidi.

2 Maana mnayajua yale maagizo tuliyowapeni kwa mamlaka ya Bwana Yesu.

3 Mungu anataka ninyi muwe watakatifu na mjiepushe kabisa na maisha ya zinaa.

4 Kila mwanamume anapaswa kujua namna ya kuishi na mkewe kwa utakatifu na heshima,

5 na si kwa tamaa mbaya kama watu wa mataifa mengine wasiomjua Mungu.

6 Basi, mtu yeyote asimkosee au kumpunja mwenzake kuhusu jambo hili. Tulikwisha waambieni hayo na kuwaonya kwamba Bwana atawaadhibu wanaofanya mambo hayo.

7 Mungu hakutuita tuishi maisha ya zinaa, bali tuishi katika utakatifu.

8 Kwa hiyo basi, anayedharau mafundisho hayo hamdharau mtu, bali amdharau Mungu mwenyewe anayewapeni Roho wake Mtakatifu.

9 Hakuna haja ya kuwaandikieni juu ya kuwapenda ndugu zenu waumini. Ninyi wenyewe mmefundishwa na Mungu namna mnavyopaswa kupendana.

10 Na mmekuwa mkiwatendea hivyo ndugu zenu wote kila mahali katika Makedonia. Basi, ndugu tunawaombeni mfanye hata zaidi.

11 Muwe na nia ya kuishi maisha ya utulivu, kila mmoja ashughulikie mambo yake mwenyewe na afanye kazi kwa mikono yake mwenyewe kama tulivyowaagiza pale awali.

12 Kwa namna hiyo mtajipatia sifa nzuri kutoka kwa wale wasio Wakristo, na hamtakuwa na lazima ya kuwategemea wengine kwa mahitaji yenu.

13 Ndugu, twataka mjue ukweli kuhusu wale ambao wamekwisha fariki dunia, ili msipatwe na huzuni kama watu wengine wasio na matumaini.

14 Sisi tunaamini kwamba Yesu alikufa, akafufuka; na hivyo sisi tunaamini kwamba Mungu atawaleta pamoja na Yesu wale wote waliofariki wakiwa wanamwamini.

15 Hili tunalowaambieni ni fundisho la Bwana; sisi tulio hai, ambao tutakuwa tumebaki, wakati Bwana atakapokuja, hakika hatutawatangulia wale waliokwisha fariki dunia.

16 Maana patatolewa amri, sauti ya malaika mkuu, sauti ya tarumbeta ya Mungu, naye Bwana mwenyewe atashuka kutoka mbinguni. Ndipo wale waliokufa wakiwa wanamwamini Kristo watafufuliwa kwanza.

17 Kisha sisi tulio hai wakati huo tutakusanywa pamoja nao katika mawingu kumlaki Bwana hewani. Na hivyo tutakuwa daima pamoja na Bwana.

18 Basi, farijianeni kwa maneno haya.