1 Ndugu, hakuna haja ya kuwaandikieni juu ya nyakati na majira yatakapotukia mambo haya.

2 Maana ninyi wenyewe mwajua kwamba Siku ya Bwana itakuja kama mwizi ajavyo usiku.

3 Watu watakapokuwa wanasema: "Kila kitu ni shwari na salama" ndipo uharibifu utakapowaangukia ghafla! Mambo hayo yatatukia ghafla kama uchungu wa uzazi unavyomjia mama anayejifungua, wala watu hawataweza kuepukana nayo.

4 Lakini ninyi ndugu, hamko gizani, na siku hiyo haipaswi kuwajieni ghafla kama vile mwizi.

5 Ninyi nyote ni watu mnaoishi katika mwanga, watu wa mchana. Sisi si watu wa usiku, wala wa giza.

6 Basi, tusilale usingizi kama wengine; tunapaswa kukesha na kuwa na kiasi.

7 Wanaolala hulala usiku, na walevi hulewa usiku.

8 Lakini sisi ni watu wa mchana na tunapaswa kuwa na kiasi. Tunapaswa kuvaa imani na upendo kama vazi la kujikinga kifuani, na tumaini letu la wokovu kama kofia ya chuma.

9 Maana Mungu hakututeua ili tuangamizwe na ghadhabu yake, bali tuupate wokovu kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo,

10 ambaye alikufa kwa ajili yetu, ili tuishi pamoja naye, iwe tu hai au tumekufa.

11 Kwa hiyo farijianeni na kusaidiana ninyi kwa ninyi kama mnavyofanya sasa.

12 Ndugu, tunawaombeni muwastahi wale wanaofanya kazi kati yenu, wale wanaowaongoza na kuwafundisheni kuhusu maisha ya Kikristo.

13 Wapeni heshima kubwa na kuwapenda kwa sababu ya kazi wanayofanya. Muwe na amani kati yenu.

14 Ndugu, tunawahimizeni muwaonye watu walio wavivu, muwatie moyo watu wanyonge, muwasaidie watu dhaifu, muwe na subira kwa wote.

15 Angalieni mtu yeyote asimlipe mwingine maovu kwa maovu, ila nia yenu iwe kutendeana mema daima na kuwatendea mema watu wote.

16 Furahini daima,

17 salini kila wakati

18 na muwe na shukrani katika kila hali. Hayo ndiyo anayotaka Mungu kwenu katika kuungana kwenu na Kristo Yesu.

19 Msimpinge Roho Mtakatifu;

20 msidharau unabii.

21 Pimeni kila kitu: zingatieni kilicho chema,

22 na epukeni kila aina ya uovu.

23 Mungu anayetupatia amani awafanye ninyi watakatifu kwa kila namna na kuzilinda nafsi zenu--roho, mioyo na miili yenu--mbali na hatia yoyote wakati wa kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo.

24 Yeye anayewaita ninyi atafanya hivyo kwani ni mwaminifu.

25 Ndugu, tuombeeni na sisi pia.

26 Wasalimuni ndugu wote kwa ishara ya upendo.

27 Nawahimizeni kwa jina la Bwana muwasomee ndugu zetu wote barua hii.

28 Tunawatakieni neema ya Bwana wetu Yesu Kristo.