11 Kisha nikaona mbingu zimefunguliwa; na huko alikuwako farasi mmoja mweupe, na mpanda farasi wake aliitwa "Mwaminifu" na "Kweli". Huyo huhukumu na kupigana kwa ajili ya haki.

12 Macho yake ni kama mwali wa moto, na alikuwa amevaa taji nyingi kichwani. Alikuwa ameandikwa jina ambalo hakuna mtu alijuaye isipokuwa tu yeye mwenyewe.

13 Alikuwa amevaa vazi lililokuwa limelowekwa katika damu. Na jina lake huyo ni "Neno la Mungu."

14 Majeshi ya mbinguni yalimfuata yakiwa yamepanda farasi weupe na walikuwa wamevaa mavazi ya kitani, meupe na safi.

15 Upanga mkali hutoka kinywani mwake, na kwa upanga huo atawashinda mataifa. Yeye ndiye atakayetawala kwa fimbo ya chuma na kuikamua divai katika chombo cha kukamulia zabibu za ghadhabu kuu ya Mungu Mwenye Uwezo.

16 Juu ya vazi lake, na juu ya mguu wake, alikuwa ameandikwa jina: "Mfalme wa wafalme na Bwana wa mabwana."