1 Kisha nikaona mbingu mpya na dunia mpya. Mbingu ile ya kwanza na dunia ile ya kwanza vilikuwa vimetoweka, nayo bahari pia haikuweko tena.
2 Nikaona mji mtakatifu, Yerusalemu mpya, ukishuka kutoka kwa Mungu mbinguni. Ulikuwa umetayarishwa vizuri kama bibi arusi aliyepambwa tayari kukutana na mumewe.
3 Kisha nikasikia sauti kubwa kutoka katika kiti cha enzi ikisema, "Tazama! Mungu amefanya makao yake kati ya watu. Atakaa kati yao, nao watakuwa watu wake, naye atakuwa Mungu wao.
4 Yeye atayafuta machozi yao yote; maana hakutakuwako tena na kifo, wala uchungu, wala kilio, wala maumivu; maana ile hali ya kale imepita!"
5 Kisha yule aliyeketi juu ya kiti cha enzi akasema, "Tazama, nafanya yote mapya." Tena akaniambia, "Andika hili, maana maneno haya ni ya kuaminika na ya kweli!"