1 Kisha malaika akanionyesha mto wa maji ya uzima maangavu kama kioo yakitoka kwenye kiti cha enzi cha Mungu na Mwanakondoo.
2 Mto huo ulitiririka kupitia katikati ya barabara kuu ya mji. Kandokando ya mto huo kulikuwa na mti wa uzima unaozaa matunda mara kumi na mbili kwa mwaka, yaani kila mwezi; na majani yake ni dawa ya kuwaponya watu wa mataifa.
3 Hapana kitu chochote kilicholaaniwa kitakachokuwa katika mji huo. Kiti cha enzi cha Mungu na cha Mwanakondoo kitakuwa katika mji huo, na watumishi wake watamwabudu.
4 Watauona uso wake, na jina lake litaandikwa juu ya paji za nyuso zao.
5 Usiku hautakuwako tena, wala hawatahitaji mwanga wa taa au wa jua, maana Bwana Mungu atawaangazia, nao watatawala milele na milele.