1 Ndugu, kama mkimwona mtu fulani amekosea, basi, ninyi mnaoongozwa na Roho mwonyeni mtu huyo ajirekebishe; lakini fanyeni hivyo kwa upole, mkiwa na tahadhari msije nanyi wenyewe mkajaribiwa.
2 Saidianeni kubeba mizigo yenu na hivyo mtatimiza sheria ya Kristo.
3 Mtu akijiona kuwa ni kitu, na kumbe si kitu, huyo anajidanganya mwenyewe.
4 Lakini kila mmoja na aupime vizuri mwenendo wake mwenyewe. Ukiwa mwema, basi, anaweza kuona fahari juu ya alichofanya bila kuwa na sababu ya kujilinganisha na mtu mwingine.
5 Maana kila mmoja anao mzigo wake mwenyewe wa kubeba.
6 Mwenye kufundishwa neno la Mungu na amshirikishe mwalimu wake riziki zake.
7 Msidanganyike; Mungu hafanyiwi dhihaka. Alichopanda mtu ndicho atakachovuna.
8 Apandaye katika tamaa za kidunia, atavuna humo uharibifu; lakini akipanda katika Roho, atavuna kutoka kwa Roho uzima wa milele.
9 Basi, tusichoke kutenda mema; maana tusipolegea tutavuna mavuno kwa wakati wake.
10 Kwa hiyo, tukiwa bado na wakati, tuwatendee watu wote mema, na hasa ndugu wa imani yetu.
11 Tazameni jinsi nilivyoandika kwa herufi kubwa, kwa mkono wangu mwenyewe.
12 Wale wanaotaka kuonekana wazuri kwa mambo ya mwili ndio wanaotaka kuwalazimisha ninyi mtahiriwe. Wanafanya hivyo kwa sababu moja tu: kusudi wao wenyewe wasije wakadhulumiwa kwa sababu ya msalaba wa Kristo.
13 Maana, hao wenyewe waliotahiriwa hawaishiki Sheria; huwataka ninyi mtahiriwe wapate kujivunia alama hiyo mwilini mwenu.
14 Lakini mimi sitajivunia kamwe chochote isipokuwa msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo; maana kwa njia ya msalaba huo ulimwengu umesulubiwa kwangu, nami nimesulubiwa kwa ulimwengu.
15 Kutahiriwa au kutotahiriwa si kitu; cha maana ni kuwa kiumbe kipya.
16 Wanaoufuata mwongozo huo nawatakia amani na huruma; amani na huruma kwa Israeli--Wateule wa Mungu.
17 Basi, sasa mtu yeyote asinisumbue tena, maana alama nilizo nazo mwilini mwangu ni zile za Yesu.
18 Ndugu, nawatakieni ninyi nyote neema ya Bwana wetu Kristo. Amina.