1 Sisi tunalo kundi hili kubwa la mashahidi mbele yetu. Kwa hiyo tuondoe kila kizuizi kinachotuzuia, na dhambi ile inayotungangania. Tupige mbio kwa uvumilivu katika mashindano yaliyowekwa mbele yetu.
2 Tumwelekee Yesu ambaye ndiye aliyeianzisha imani yetu na ambaye ataikamilisha. Kwa ajili ya furaha iliyokuwa inamngojea, yeye alivumilia kifo msalabani, bila kujali juu ya aibu yake, na sasa anaketi upande wa kulia wa kiti cha enzi cha Mungu.
3 Fikirini juu ya mambo yaliyompata Yesu, jinsi alivyostahimili upinzani mkubwa kwa watu wenye dhambi. Basi, msife moyo, wala msikate tamaa.