8 Lakini Mungu aliwalaumu watu wake aliposema: "Siku zinakuja, asema Bwana, ambapo nitafanya agano jipya na watu wa Israeli na kabila la Yuda.
9 Agano hili halitakuwa kama lile nililofanya na babu zao siku ile nilipowaongoza kwa mkono kutoka nchi ya Misri. Hawakuwa waaminifu kwa agano langu; na hivyo mimi sikuwajali, asema Bwana.
10 Na hili ndilo agano nitakalofanya na watu wa Israeli siku zijazo, asema Bwana: Nitaweka sheria zangu akilini mwao, na kuziandika mioyoni mwao. Mimi nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu.
11 Hakuna mtu atakayemfundisha mwananchi mwenzake, wala atakayemwambia ndugu yake: Mjue Bwana. Maana watu wote, wadogo na wakubwa, watanijua mimi.
12 Nitawasamehe makosa yao, wala sitakumbuka tena dhambi zao."