16 Kwa kawaida wosia hutambuliwa tu kama kifo cha yule aliyeufanya huo wosia kimethibitishwa.

17 Wosia hauwezi kutekelezwa mpaka kumetokea kifo, kwani wosia hauna maana ikiwa mwenye kuufanya bado anaishi.

18 Ndiyo maana hata lile agano la kwanza halikuwekwa bila damu kumwagwa.

19 Kwanza Mose aliwatangazia watu wote amri zote kama ilivyokuwa katika Sheria; kisha akachukua damu ya ndama pamoja na maji, na kwa kutumia majani ya mti uitwao husopo na pamba nyekundu, akakinyunyizia kile kitabu cha Sheria na hao watu wote.

20 Mose alisema: "Hii ni damu inayothibitisha agano mliloamriwa na Mungu mlitii."