1 Mtu mmoja aitwaye Lazaro, mwenyeji wa Bethania, alikuwa mgonjwa. (Kijiji cha Bethania kilikuwa mahali walipokaa Maria na Martha, dada yake.
2 Maria ndiye yule aliyempaka Bwana marashi na kumpangusa kwa nywele zake. Lazaro, kaka yake, ndiye aliyekuwa mgonjwa.)
3 Basi, hao dada wakatuma ujumbe huu kwa Yesu: "Bwana, rafiki yako ni mgonjwa!"
4 Yesu aliposikia hivyo akasema, "Ugonjwa huo hautaleta kifo, ila ni kwa ajili ya kumtukuza Mungu; ameugua ili kwa njia hiyo Mwana wa Mungu atukuzwe."
5 Yesu aliwapenda Martha, dada yake na Lazaro.
6 Alipopata habari kwamba Lazaro ni mgonjwa, Yesu aliendelea kukaa mahali hapo alipokuwa kwa siku mbili zaidi.
7 Kisha akawaambia wanafunzi wake, "Twendeni tena Yudea!"
8 Wanafunzi wakamwambia, "Mwalimu! Muda mfupi tu umepita tangu Wayahudi walipotaka kukuua kwa mawe, nawe unataka kwenda huko tena?"
9 Yesu akajibu, "Je, saa za mchana si kumi na mbili? Basi, mtu akitembea mchana hawezi kujikwaa kwa kuwa anauona mwanga wa ulimwengu huu.
10 Lakini mtu akitembea usiku atajikwaa kwa maana mwanga haumo ndani yake."
11 Yesu alipomaliza kusema maneno hayo, akawaambia, "Rafiki yetu Lazaro amelala, lakini mimi nitakwenda kumwamsha."
12 Wanafunzi wake wakamwambia, "Bwana, ikiwa amelala, basi atapona."
13 Wao walidhani kwamba alikuwa amesema juu ya kulala usingizi, kumbe alikuwa amesema juu ya kifo cha Lazaro.
14 Basi, Yesu akawaambia waziwazi, "Lazaro amekufa;