1 Baada ya hayo kulikuwa na sikukuu ya Wayahudi, naye Yesu akaenda Yerusalemu.
2 Huko Yerusalemu, karibu na mlango uitwao Mlango wa Kondoo, kulikuwa na bwawa la maji liitwalo kwa Kiebrania Bethzatha, ambalo lilikuwa na baraza tano zenye matao.
3 Humo barazani mlikuwa na wagonjwa wengi wamekaa: vipofu, viwete na waliopooza.*fa*
4 maana mara kwa mara malaika alishuka majini nyakati fulani na kuyatibua. Mtu yeyote aliyekuwa wa kwanza kuingia majini baada ya maji kutibuliwa, alipona ugonjwa wowote aliokuwa nao.
5 Basi, hapo palikuwa na mtu mmoja aliyekuwa mgonjwa kwa muda wa miaka thelathini na minane.
6 Naye alipomwona huyo mtu amelala hapo, akatambua kwamba alikuwa amekaa hapo kwa muda mrefu, akamwuliza, "Je, wataka kupona?"
7 Naye akajibu, "Mheshimiwa, mimi sina mtu wa kunipeleka majini wakati yanapotibuliwa. Kila nikijaribu kuingia, mtu mwingine hunitangulia."
8 Yesu akamwambia, "Inuka, chukua mkeka wako utembee."
9 Mara huyo mtu akapona, akachukua mkeka wake, akatembea. Jambo hili lilifanyika siku ya Sabato.