15 Basi, akawaambia wote, "Jihadharini na kila aina ya tamaa; maana uzima wa mtu hautegemei wingi wa vitu alivyo navyo."
16 Kisha akawaambia mfano: "Kulikuwa na tajiri mmoja ambaye shamba lake lilizaa mavuno mengi.
17 Tajiri huyo akafikiri moyoni mwake: Nitafanyaje nami sina mahali pa kuhifadhia mavuno yangu?
18 Nitafanya hivi: nitabomoa ghala zangu na kujenga kubwa zaidi, na humo nitahifadhi mavuno yangu yote na mali yangu.
19 Hapo nitaweza kuiambia roho yangu: sasa unayo akiba ya matumizi kwa miaka na miaka. Ponda mali, ule, unywe na kufurahi.
20 Lakini Mungu akamwambia: Mpumbavu wewe; leo usiku roho yako itachukuliwa. Na vitu vile vyote ulivyojilundikia vitakuwa vya nani?"
21 Yesu akamaliza kwa kusema "Ndivyo ilivyo kwa mtu anayejilundikia mali kwa ajili yake mwenyewe, lakini si tajiri mbele ya Mungu."