10 Yesu alikuwa akifundisha katika sunagogi moja siku ya Sabato.
11 Na hapo palikuwa na mwanamke mmoja aliyekuwa mgonjwa kwa miaka kumi na minane kutokana na pepo aliyekuwa amempagaa. Kwa sababu hiyo, mwili wake ulikuwa umepindika vibaya hata asiweze kusimama wima.
12 Yesu alipomwona, alimwita, akamwambia, "Mama, umeponywa ugonjwa wako."
13 Akamwekea mikono, na mara mwili wake ukawa wima tena, akawa anamtukuza Mungu.
14 Lakini mkuu wa sunagogi alikasirika kwa sababu Yesu alikuwa amemponya siku ya Sabato. Hivyo akawaambia wale watu walikusanyika pale, "Mnazo siku sita za kufanya kazi. Basi, fikeni siku hizo mkaponywe magonjwa yenu; lakini msije siku ya Sabato."
15 Hapo Bwana akamjibu, "Enyi wanafiki! Nani kati yenu hangemfungua ngombe au punda wake kutoka zizini ampeleke kunywa maji, hata kama siku hiyo ni ya Sabato?
16 Sasa, hapa yupo binti wa Abrahamu ambaye Shetani alimfanya kilema kwa muda wa miaka kumi na minane. Je, haikuwa vizuri kumfungulia vifungo vyake siku ya Sabato?"
17 Alipokwisha sema hayo, wapinzani wake waliona aibu lakini watu wengine wote wakajaa furaha kwa sababu ya mambo yote aliyotenda.