11 Yesu akiwa safarini kwenda Yerusalemu alipitia mipakani mwa Samaria na Galilaya.
12 Alipokuwa anaingia katika kijiji kimoja, watu kumi wenye ukoma walikutana naye, wakasimama kwa mbali.
13 Wakapaza sauti wakisema, "Yesu Mwalimu, tuonee huruma!"
14 Alipowaona akawaambia, "Nendeni mkajionyeshe kwa makuhani." Basi, ikawa walipokuwa wanakwenda, wakatakasika.
15 Mmoja wao alipoona kwamba ameponywa alirudi akimtukuza Mungu kwa sauti kubwa.
16 Akajitupa chini mbele ya miguu ya Yesu huku akimshukuru. Huyo alikuwa Msamaria.
17 Hapo Yesu akasema, "Je, si watu kumi walitakaswa? Wale tisa wako wapi?
18 Hakupatikana mwingine aliyerudi kumtukuza Mungu ila tu huyu mgeni?"
19 Halafu akamwambia huyo mtu, "Simama, uende zako; imani yako imekuponya."