1 Yesu aliingia mjini Yeriko, akawa anapita katika njia za mji huo.

2 Kulikuwa na mtu mmoja mjini, jina lake Zakayo ambaye alikuwa mkuu wa watoza ushuru tena mtu tajiri.

3 Alitaka kuona Yesu alikuwa nani, lakini kwa sababu ya umati wa watu, na kwa vile alikuwa mfupi, hakufaulu.

4 Hivyo, alitangulia mbio, akapanda juu ya mkuyu ili aweze kumwona Yesu, kwa maana alikuwa apitie hapo.

5 Basi, Yesu alipofika mahali pale, aliangalia juu akamwambia, "Zakayo, shuka upesi, maana leo ni lazima nishinde nyumbani mwako."

6 Zakayo akashuka haraka, akamkaribisha kwa furaha.

7 Watu wote walipoona hayo, wakaanza kunungunika wakisema, "Amekwenda kukaa kwa mtu mwenye dhambi."

8 Lakini Zakayo akasimama akamwambia Yesu, "Sikiliza Bwana! Mimi nitawapa maskini nusu ya mali yangu, na kama nimenyanganya mtu yeyote kitu, nitamrudishia mara nne."

9 Yesu akamwambia, "Leo wokovu umefika katika nyumba hii, kwa vile huyu pia ni wa ukoo wa Abrahamu.

10 Kwa maana Mwana wa Mtu amekuja kutafuta na kuokoa waliopotea." ic