1 Siku zile, tangazo rasmi lilitolewa na Kaisari Augusto kuwataka watu wote chini ya utawala wake wajiandikishe.

2 Kuandikishwa huku kulikuwa mara ya kwanza, wakati Kirenio alipokuwa mkuu wa mkoa wa Siria.

3 Basi, wote waliohusika walikwenda kujiandikisha, kila mtu katika mji wake.

4 Yosefu pia alifanya safari kutoka mjini Nazareti mkoani Galilaya. Kwa kuwa alikuwa wa jamaa na ukoo wa Daudi alikwenda mjini Bethlehemu mkoani Yuda alikozaliwa Mfalme Daudi.

5 Alikwenda kujiandikisha pamoja na mchumba wake Maria ambaye alikuwa mja mzito.