33 Walipofika mahali paitwapo, "Fuvu la Kichwa," ndipo wakamsulubisha Yesu pamoja na wale wahalifu wawili, mmoja upande wake wa kulia na mwingine upande wake wa kushoto.
34 Yesu akasema, "Baba, uwasamehe kwa maana hawajui wanalofanya." Kisha wakagawana mavazi yake kwa kuyapigia kura.
35 Watu wakawa wamesimama pale wakitazama. Nao viongozi wakamdhihaki wakisema: "Amewaokoa wengine; sasa na ajiokoe mwenyewe, kama yeye ndiye Kristo, mteule wa Mungu!"
36 Askari nao walimdhihaki pia; walimwendea wakampa siki
37 wakisema: "Kama kweli wewe ni Mfalme wa Wayahudi, jiokoe mwenyewe."
38 Vilevile maandishi haya yalikuwa yameandikwa na kuwekwa juu yake: "Huyu ndiye Mfalme wa Wayahudi."
39 Mmoja wa wale wahalifu waliotundikwa msalabani, alimtukana akisema: "Je, si kweli kwamba wewe ndiwe Kristo? Basi, jiokoe mwenyewe, utuokoe na sisi pia."
40 Lakini yule mhalifu mwingine akamkemea mwenzake akisema: "Wewe humwogopi Mungu hata kidogo? Wewe umepata adhabu hiyohiyo.
41 Wewe na mimi tunastahili, maana haya ni malipo ya yale tuliyotenda. Lakini mtu huyu hakufanya chochote kibaya."
42 Kisha akasema, "Ee Yesu! Unikumbuke wakati utakapoingia katika ufalme wako."
43 Yesu akamwambia, "Nakwambia kwa hakika, leo utakuwa pamoja nami peponi."