1 Siku moja Yesu alikuwa amesimama kando ya ziwa Genesareti, na watu wengi walikuwa wamemzunguka wakisongana wanalisikiliza neno la Mungu.
2 Akaona mashua mbili ukingoni mwa ziwa; wavuvi wenyewe walikuwa wametoka, wanaosha nyavu zao.
3 Baada ya Yesu kuingia katika mashua moja, iliyokuwa ya Simoni, alimtaka Simoni aisogeze majini, mbali kidogo na ukingo wa ziwa. Akaketi, akafundisha umati wa watu akiwa ndani ya mashua.
4 Alipomaliza kufundisha, akamwambia Simoni, "Peleka mashua mpaka kilindini, mkatupe nyavu zenu mpate kuvua samaki."
5 Simoni akamjibu, "Bwana, tumejitahidi kuvua samaki usiku kucha bila kupata kitu, lakini kwa kuwa umesema, nitatupa nyavu."
6 Baada ya kufanya hivyo, wakavua samaki wengi, hata nyavu zao zikaanza kukatika.
7 Wakawaita wenzao waliokuwa katika mashua nyingine waje kuwasaidia. Wakaja, wakazijaza mashua zote mbili samaki, hata karibu zingezama.
8 Simoni Petro alipoona hayo, akapiga magoti mbele ya Yesu akisema, "Ondoka mbele yangu, ee Bwana, kwa kuwa mimi ni mwenye dhambi!"
9 Simoni pamoja na wenzake wote walishangaa kwa kupata samaki wengi vile.
10 Hali kadhalika Yakobo na Yohane, wana wa Zebedayo, waliokuwa wavuvi wenzake Simoni. Yesu akamwambia Simoni, "Usiogope; tangu sasa utakuwa ukivua watu."
11 Basi, baada ya kuzileta zile mashua ukingoni mwa ziwa, wakaacha yote, wakamfuata.