1 Baada ya kusema yale aliyotaka watu wasikie, Yesu alikwenda Kafarnaumu.
2 Huko kulikuwa na jemadari mmoja Mroma ambaye alikuwa na mtumishi wake aliyempenda sana. Huyu mtumishi alikuwa mgonjwa karibu kufa.
3 Yule jemadari aliposikia habari za Yesu, aliwatuma wazee fulani Wayahudi waende kumwomba aje amponye mtumishi wake.
4 Walipofika kwa Yesu, walimsihi sana, wakasema: "Huyu anastahili afanyiwe jambo hilo,
5 maana analipenda taifa letu, na ndiye aliyetujengea lile sunagogi."
6 Basi, Yesu akaenda pamoja nao. Alipokuwa karibu kufika nyumbani kwa yule jemadari Mroma, yule jemadari aliwatuma marafiki zake wamwambie Yesu: "Bwana, usijisumbue zaidi, maana mimi sistahili uingie nyumbani mwangu.
7 Ndio maana sikujiona nastahili hata kuja kwako; amuru tu, na mtumishi wangu atapona.
8 Mimi pia ni mtu niliye chini ya mamlaka, na ninao askari chini yangu. Namwambia mmoja, `Nenda!`, naye huenda; namwambia mwingine, `Njoo!` naye huja; na nikimwambia mtumishi wangu, `Fanya hiki!`, hufanya."
9 Yesu aliposikia hayo, alishangaa; halafu akauelekea ule umati wa watu uliokuwa unamfuata, akasema, "Sijaona imani kubwa namna hii hata katika Israeli."
10 Wale watu walipowasili nyumbani walimkuta yule mtumishi hajambo kabisa.
11 Baadaye kidogo Yesu alikwenda katika mji mmoja uitwao Naini, na wafuasi wake pamoja na kundi kubwa la watu waliandamana naye.
12 Basi, alipokuwa anakaribia lango la mji, walitokea watu wamebeba maiti ya kijana mmoja, mtoto wa pekee wa mama mjane. Watu wengi wa mji ule walikuwa pamoja na huyo mama.
13 Bwana alipomwona mama huyo, alimwonea huruma, akamwambia, "Usilie."
14 Kisha akaenda, akaligusa lile jeneza, na wale waliokuwa wanalichukua wakasimama. Halafu akasema, "Kijana! Nakuamuru, amka!"
15 Yule aliyekufa akaketi, akaanza kuongea. Na Yesu akamkabidhi kwa mama yake.
16 Watu wote walishikwa na hofu, wakawa wanamtukuza Mungu wakisema: "Nabii mkuu ametokea kati yetu. Mungu amekuja kuwakomboa watu wake."
17 Habari hizo zikaenea kote katika Uyahudi na katika nchi za jirani.
18 Wanafunzi wa Yohane walimpa habari Yohane juu ya mambo hayo yote. Naye Yohane, baada ya kuwaita wawili kati ya wanafunzi wake,
19 aliwatuma kwa Bwana wamwulize: "Wewe ndiye yule ajaye, au tumtazamie mwingine?"
20 Wale wanafunzi walipomfikia Yesu wakamwambia, "Yohane Mbatizaji ametutuma kwako tukuulize: `Wewe ndiye yule ajaye, au tumtazamie mwingine?"`
21 Wakati huohuo, Yesu alikuwa anawaponya watu wengi waliokuwa wanateseka kwa magonjwa na waliopagawa na pepo wabaya, akawawezesha vipofu wengi kuona tena.
22 Basi, Yesu akawajibu, "Nendeni mkamwambie Yohane yale mliyojionea na kuyasikia: vipofu wanaona, viwete wanatembea, wenye ukoma wanatakaswa, viziwi wanasikia, wafu wanafufuliwa, na maskini wanahubiriwa Habari njema.
23 Heri mtu yule ambaye hana mashaka nami!"
24 Hapo wajumbe wa Yohane walipokwisha kwenda zao, Yesu alianza kuyaambia makundi ya watu juu ya Yohane: "Mlikwenda kule jangwani, hivi mlitaka kuona kitu gani? Mlitaka kuona unyasi unaotikiswa na upepo?
25 Basi, mlikwenda kuona nini? Mlikwenda kumwona mtu aliyevalia mavazi maridadi? La hasha! Wanaovaa mavazi maridadi na kuishi maisha ya anasa, hukaa katika majumba ya wafalme!
26 Basi, niambieni, mlikwenda kuona nini? Mlikwenda kumwona nabii? Naam, hakika ni zaidi ya nabii.
27 Huyu Yohane ndiye anayesemwa katika Maandiko Matakatifu: `Hapa ni mtumishi wangu, asema Bwana; ninamtuma akutangulie, akutayarishie njia."`
28 Yesu akamalizia kwa kusema, "Nawaambieni, kati ya binadamu wote hakuna aliye mkubwa zaidi kuliko Yohane Mbatizaji. Hata hivyo, yule aliye mdogo kabisa katika ufalme wa Mungu ni mkubwa zaidi kuliko yeye."
29 Waliposikia hayo watu wote na watoza ushuru waliusifu wema wa Mungu; hao ndio wale waliokuwa wameupokea ubatizo wa Yohane.
30 Lakini Mafarisayo na walimu wa Sheria walikataa mpango wa Mungu uliowahusu wakakataa kubatizwa na Yohane.
31 Yesu akaendelea kusema, "Basi, nitawafananisha watu wa kizazi hiki na kitu gani? Ni watu wa namna gani?
32 Ni kama vijana waliokuwa wamekaa sokoni na kuambiana, kikundi kimoja na kingine: `Tumewapigieni ngoma, lakini hamkucheza! Tumeomboleza, lakini hamkulia!`
33 Kwa maana Yohane alikuja, yeye alifunga na hakunywa divai, nanyi mkasema: `Amepagawa na pepo!`
34 Akaja Mwana wa Mtu; anakula na kunywa, mkasema: `Mwangalieni mlafi huyu na mlevi; rafiki ya watoza ushuru na wenye dhambi!`
35 Hata hivyo, hekima ya Mungu imethibitishwa kuwa njema na wote wale wanaoikubali."
36 Mfarisayo mmoja alimwalika Yesu kula chakula nyumbani kwake. Akaingia nyumbani mwa huyo Mfarisayo, akakaa kula chakula.
37 Basi, katika mji ule kulikuwa na mama mmoja aliyekuwa anaishi maisha mabaya. Alipopata habari kwamba Yesu yuko nyumbani kwa huyo Mfarisayo, alichukua chupa ya alabasta yenye marashi.
38 Akaja, akasimama karibu na miguu yake Yesu, akilia, na machozi yake yakamdondokea Yesu miguuni. Huyo mwanamke akaipangusa miguu ya Yesu kwa nywele zake. Kisha akaibusu na kuipaka yale marashi.
39 Yule Mfarisayo aliyemwalika Yesu alipoona hayo, akawaza moyoni mwake, "Kama mtu huyu angekuwa kweli nabii angejua huyu mwanamke ni wa namna gani, ya kwamba ni mwenye dhambi."
40 Yesu akamwambia huyo Mfarisayo, "Simoni, ninacho kitu cha kukwambia." Naye Simoni akamwambia, "Ndio Mwalimu, sema." Yesu akasema,
41 "Watu wawili walikuwa wamemkopa mtu fedha: mmoja alikuwa amekopa dinari mia tano, na mwingine hamsini.
42 Waliposhindwa kulipa madeni yao, huyo mtu aliwasamehe wote wawili. Sasa ni yupi kati ya hao wawili atampenda zaidi huyo bwana?"
43 Simoni akamjibu, "Ni dhahiri kwamba yule aliyesamehewa deni kubwa zaidi atampenda zaidi yule bwana." Yesu akamwambia, "Sawa."
44 Halafu akamgeukia yule mwanamke na kumwambia Simoni, "Unamwona huyu mwanamke, sivyo? Basi, mimi nilipoingia hapa nyumbani kwako hukunipa maji ya kunawa miguu yangu; lakini mwanamke huyu ameniosha miguu yangu kwa machozi yake na kunipangusa kwa nywele zake.
45 Wewe hukunisalimu kwa kunibusu, lakini huyu mwanamke tangu nilipoingia hapa amekuwa akiibusu miguu yangu.
46 Wewe hukunionyesha ukarimu wako kwa kunipaka mafuta kichwani, lakini huyu mwanamke amefanya hivyo kwa kunipaka mafuta miguu yangu.
47 Kwa hiyo nakwambia amesamehewa dhambi zake nyingi kwa kuwa ameonyesha upendo mkubwa. Mwenye kusamehe kidogo, hupenda kidogo."
48 Basi, Yesu akamwambia yule mwanamke, "Umesamehewa dhambi zako."
49 Na hapo wale waliokuwa pamoja naye mezani wakaulizana, "Ni mtu wa namna gani huyu awezaye kusamehe dhambi?"
50 Naye Yesu akamwambia yule mwanamke, "Imani yako imekuokoa; nenda kwa amani."