1 Walipokuwa wanakaribia Yerusalemu walifika Bethfage na Bethania, karibu na mlima wa Mizeituni. Hapo aliwatuma wawili wa wanafunzi wake,
2 akawaambia, "Nendeni katika kijiji kilicho mbele yenu. Mtakapokuwa mnaingia humo, mtakuta mwana punda amefungwa ambaye bado hajatumiwa na mtu. Mfungueni mkamlete.
3 Kama mtu akiwauliza, Mbona mnafanya hivyo? Mwambieni, Bwana anamhitaji na atamrudisha hapa mara." ic\is Bethania (Marko 11:1)\ie
4 Basi, wakaenda, wakamkuta mwana punda barabarani amefungwa mlangoni. Walipokuwa wakimfungua,
5 baadhi ya watu waliokuwa wamesimama hapo wakawauliza "Kwa nini mnamfungua huyo mwana punda?"
6 Wanafunzi wakajibu kama Yesu alivyokuwa amewaambia; nao wakawaacha waende zao.
7 Wakampelekea Yesu huyo mwana punda. Wakatandika mavazi yao juu ya huyo mwana punda, na Yesu akaketi juu yake.
8 Watu wengi wakatandaza mavazi yao barabarani; wengine wakatandaza matawi ya miti waliyoyakata mashambani.
9 Watu wote waliotangulia na wale waliofuata wakapaaza sauti zao wakisema, "Hosana! Abarikiwe huyo ajaye kwa jina la Bwana!
10 Ubarikiwe Ufalme ujao wa baba yetu Daudi. Hosana juu mbinguni!"
11 Yesu aliingia mjini Yerusalemu akaenda moja kwa moja mpaka Hekaluni, akatazama kila kitu kwa makini. Lakini kwa vile ilikwisha kuwa jioni, akaenda Bethania pamoja na wale kumi na wawili.