1 Basi, wakafika katika nchi ya Wagerase, ngambo ya ziwa.

2 Mara tu Yesu aliposhuka mashuani, mtu mmoja aliyepagawa na pepo mchafu alitoka makaburini, akakutana naye.

3 Mtu huyo alikuwa akiishi makaburini wala hakuna mtu aliyeweza tena kumfunga kwa minyororo.

4 Mara nyingi walimfunga kwa pingu na minyororo lakini kila mara aliweza kuikata hiyo minyororo na kuzivunja hizo pingu, wala hakuna mtu aliyeweza kumzuia.

5 Mchana na usiku alikaa makaburini na milimani akipaaza sauti na kujikatakata kwa mawe.

6 Alipomwona Yesu kwa mbali, alimkimbilia, akamwinamia

7 akisema kwa sauti kubwa, "Una shauri gani nami, wewe Yesu Mwana wa Mungu aliye juu? Kwa jina la Mungu, nakusihi usinitese!"

8 Alisema hivyo kwa kuwa Yesu alikuwa amemwambia, "Pepo mchafu, mtoke mtu huyu.")

9 Basi, Yesu akamwuliza, "Jina lako nani?" Naye akajibu, "Jina langu ni Jeshi, maana sisi tu wengi."

10 Kisha akamsihi Yesu asiwafukuze hao pepo katika nchi ile.

11 Kulikuwa na kundi kubwa la nguruwe malishoni kwenye mteremko wa mlima.

12 Basi, hao pepo wakamsihi, "Utupeleke kwa hao nguruwe, tuwaingie."

13 Naye akawaruhusu. Basi, hao pepo wachafu wakatoka, wakawaingia wale nguruwe. Kundi lote la nguruwe wapatao elfu mbili likaporomoka kwenye ule mteremko mkali mpaka ziwani, likatumbukia majini.

14 Wachungaji wa hao nguruwe walikimbia, wakatangaza jambo hilo mjini na mashambani. Watu wakafika kuona yaliyotukia.