1 Baada ya siku sita, Yesu aliwachukua Petro, Yakobo na Yohane nduguye, akaenda nao peke yao juu ya mlima mrefu.

2 Huko, wakiwa wanamtazama, akageuka sura, uso wake ukangaa kama jua na mavazi yake yakawa meupe kama nuru.

3 Mose na Eliya wakawatokea, wakawa wanazungumza naye.

4 Hapo Petro akamwambia Yesu, "Bwana, ni vizuri sana kwamba tupo hapa! Ukipenda nitajenga vibanda vitatu: kimoja chako, kimoja cha Mose na kimoja cha Eliya."

5 Alipokuwa bado anasema hivyo, wingu jeupe likawafunika, na sauti ikasikika kutoka katika hilo wingu: "Huyu ni Mwanangu mpendwa, ninayependezwa naye, msikilizeni."