21 Kisha Petro akamwendea Yesu, akamwuliza, "Je, ndugu yangu akinikosea, nimsamehe mara ngapi? Mara saba?"
22 Yesu akamjibu, "Sisemi mara saba tu, bali sabini mara saba.
23 Ndiyo maana Ufalme wa mbinguni umefanana na mfalme mmoja aliyeamua kukagua hesabu za watumishi wake.
24 Ukaguzi ulipoanza, akaletewa mtu mmoja aliyekuwa na deni la fedha talanta elfu kumi.
25 Mtu huyo hakuwa na chochote cha kulipa; hivyo bwana wake aliamuru wauzwe, yeye, mke wake, watoto wake na vitu vyote alivyokuwa navyo, ili deni lilipwe.
26 Basi, huyo mtumishi akapiga magoti mbele yake, akasema, Unisubiri nami nitakulipa deni lote.
27 Yule bwana alimwonea huruma, akamsamehe lile deni, akamwacha aende zake.
28 "Lakini huyo mtumishi akaondoka, akamkuta mmoja wa watumishi wenzake aliyekuwa na deni lake fedha denari mia moja. Akamkamata, akamkaba koo akisema, Lipa deni lako!
29 Huyo mtumishi mwenzake akapiga magoti, akamwomba, Unisubiri nami nitalipa deni langu lote.
30 Lakini yeye hakutaka, bali alimtia gerezani mpaka hapo atakapolipa lile deni.
31 "Basi, watumishi wenzake walipoona jambo hilo walisikitika sana, wakaenda kumpasha habari bwana wao juu ya mambo hayo yaliyotukia.
32 Hapo yule bwana alimwita huyo mtumishi, akamwambia, Wewe ni mtumishi mbaya sana! Uliniomba, nami nikakusamehe deni lako lote.
33 Je, haikukupasa nawe kumhurumia mtumishi mwenzako kama nilivyokuhurumia?
34 "Basi, huyo bwana alikasirika sana, akamtoa huyo mtumishi aadhibiwe mpaka hapo atakapolipa deni lote.
35 Na baba yangu aliye mbinguni atawafanyieni vivyo hivyo kama kila mmoja wenu hatamsamehe ndugu yake kwa moyo wake wote."