1 Yesu na wanafunzi wake walipokaribia Yerusalemu na kufika Bethfage katika mlima wa Mizeituni, aliwatuma wanafunzi wake wawili,

2 akawaambia, "Nendeni hadi kijiji kilicho mbele yenu na mtamkuta punda amefungwa na mtoto wake. Wafungueni mkawalete kwangu.

3 Kama mtu akiwauliza sababu, mwambieni, Bwana anawahitaji, naye atawaachieni mara."

4 Jambo hili lilifanyika ili yale yaliyosemwa na nabii yatimie:

5 "Uambieni mji wa Sioni: Tazama, Mfalme wako anakujia! Ni mpole na amepanda punda, mwana punda, mtoto wa punda."

6 Hivyo, wale wanafunzi walienda wakafanya kama Yesu alivyowaagiza.

7 Wakamleta yule punda na mtoto wake, wakatandika nguo zao juu yao na Yesu akaketi juu yake.

8 Umati mkubwa wa watu ukatandaza nguo zao barabarani, na watu wengine wakakata matawi ya miti wakayatandaza barabarani.

9 Makundi ya watu waliomtangulia na wale waliomfuata wakapaaza sauti: "Hosana Mwana wa Daudi! Abarikiwe huyo ajaye kwa jina la Bwana! Hosana Mungu juu mbinguni!"

10 Yesu alipokuwa anaingia Yerusalemu, mji wote ukajaa ghasia. Watu wakawa wanauliza, "Huyu ni nani?"

11 Watu katika ule umati wakasema, "Huyu ni nabii Yesu, kutoka Nazareti katika mkoa wa Galilaya."