1 Yesu alipomaliza kusema hayo yote, aliwaambia wanafunzi wake,

2 "Mnajua kwamba baada ya siku mbili tutakuwa na sikukuu ya Pasaka, na Mwana wa Mtu atatolewa ili asulubiwe."

3 Wakati huo makuhani wakuu na wazee wa watu walikutana pamoja katika ukumbi wa Kayafa, Kuhani Mkuu.

4 Wakashauriana jinsi ya kumtia Yesu nguvuni kwa hila wamuue.

5 Lakini wakaamua jambo hilo lisifanyike wakati wa sikukuu, kusije kukatokea ghasia kati ya watu.

6 Yesu alipokuwa Bethania, nyumbani kwa Simoni, aitwaye Mkoma,

7 mama mmoja aliyekuwa na chupa ya alabasta yenye marashi ya thamani kubwa, alimjia pale mezani alipokuwa amekaa kula chakula, akammiminia hayo marashi kichwani.

8 Wanafunzi wake walipoona hayo wakakasirika, wakasema, "Ya nini hasara hii?

9 Marashi haya yangaliweza kuuzwa kwa bei kubwa, maskini wakapewa hizo fedha."

10 Yesu alitambua mawazo yao, akawaambia, "Mbona mnamsumbua huyu mama? Yeye amenitendea jambo jema.

11 Maskini mnao daima pamoja nanyi, lakini mimi sitakuwapo pamoja nanyi daima.

12 Huyu mama amenimiminia marashi ili kunitayarisha kwa maziko.

13 Nawaambieni kweli, popote ambapo hii Habari Njema itahubiriwa ulimwenguni, kitendo hiki alichofanya mama huyu kitatajwa kwa kumkumbuka yeye."

14 Kisha, Yuda Iskarioti, mmoja wa wale kumi na wawili, akaenda kwa makuhani wakuu,

15 akawaambia, "Mtanipa kitu gani kama nikimkabidhi Yesu kwenu?" Wakamhesabia sarafu thelathini za fedha;

16 na tangu wakati huo Yuda akawa anatafuta nafasi ya kumsaliti.

17 Siku ya kwanza kabla ya Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu, wanafunzi walimwendea Yesu wakamwuliza, "Unataka tukuandalie wapi chakula cha Pasaka?"

18 Yeye akawajibu, "Nendeni mjini kwa mtu fulani, mkamwambie: Mwalimu anasema, wakati wangu umefika; kwako nitakula Pasaka pamoja na wanafunzi wangu."

19 Wanafunzi wakafanya kama Yesu alivyowaagiza, wakaandaa Pasaka.

20 Kulipokuwa jioni, Yesu akakaa mezani pamoja na wanafunzi wake kumi na wawili.

21 Walipokuwa wakila, Yesu akasema, "Nawaambieni kweli, mmoja wenu atanisaliti."

22 Wanafunzi wakahuzunika sana, wakaanza kuuliza mmojammoja, "Bwana! Je, ni mimi?"

23 Yesu akajibu, "Atakayechovya mkate pamoja nami katika bakuli ndiye atakayenisaliti.*fm*

24 Naam, Mwana wa Mtu anakwenda zake kama Maandiko Matakatifu yasemavyo, lakini ole wake mtu yule atakayemsaliti Mwana wa Mtu! Ingalikuwa afadhali kwa mtu huyo kama hangalizaliwa."

25 Yuda, ambaye ndiye aliyetaka kumsaliti, akamwuliza, "Mwalimu! Je, ni mimi?" Yesu akamjibu, "Wewe umesema."

26 Walipokuwa wanakula, Yesu akatwaa mkate, akashukuru, akaumega, akawapa wanafunzi wake akisema, "Twaeni mle; huu ni mwili wangu."

27 Kisha akatwaa kikombe, akamshukuru Mungu, akawapa akisema, "Nyweni nyote;

28 maana hii ni damu yangu inayothibitisha agano,*fn* damu inayomwagwa kwa ajili ya watu wengi ili kuwaondolea dhambi.