19 Hekalu la Mungu mbinguni likafunguliwa, na Sanduku la Agano lake likaonekana Hekaluni mwake. Kisha kukatokea umeme, sauti, ngurumo, tetemeko la ardhi, na mvua kubwa ya mawe.
1 Agano la kwanza lilikuwa na taratibu zake za ibada na pia mahali patakatifu pa ibada palipojengwa na watu.
2 Palitengenezwa hema ambayo sehemu yake ya nje iliitwa Mahali Patakatifu. Humo mlikuwa na kinara cha taa, meza na mikate iliyotolewa kwa Mungu.
3 Nyuma ya pazia la pili, kulikuwa na hema iliyoitwa Mahali Patakatifu Kupita Pote.
4 Humo mlikuwa na madhabahu ya dhahabu kwa ajili ya kufukizia ubani, na Sanduku la Agano, ambalo lilikuwa limepakwa dhahabu pande zote, na ndani yake mlikuwa na chungu cha dhahabu kilichokuwa na mana; fimbo ya Aroni iliyokuwa imechanua majani, na vile vibao viwili vilivyoandikwa agano.
5 Juu ya hilo Sanduku kulikuwa na viumbe vilivyodhihirisha kuweko kwa Mungu, na mabawa yao yalitanda juu ya mahali ambapo dhambi huondolewa. Lakini sasa, hatuwezi kusema kinaganaga juu ya mambo hayo.