17 Katika siku zile za mwisho, asema Bwana, nitawamiminia binadamu wote Roho wangu. Watoto wenu, wanaume kwa wanawake, watautangaza ujumbe wangu; vijana wenu wataona maono, na wazee wenu wataota ndoto.
18 Naam, hata watumishi wangu, wanaume kwa wanawake, nitawamiminia Roho wangu, siku zile, nao watautangaza ujumbe wangu.
19 Nitatenda miujiza juu angani, na ishara chini duniani; kutakuwa na damu, moto na moshi mzito;
20 jua litatiwa giza, na mwezi utakuwa mwekundu kama damu, kabla ya kutokea ile siku kuu na tukufu ya Bwana.
21 Hapo, yeyote atakayeomba kwa jina la Bwana, ataokolewa.
51 Sikilizeni, nawaambieni siri: sisi hatutakufa sote, ila sote tutageuzwa
52 wakati wa mbiu ya mwisho, kwa nukta moja, kufumba na kufumbua. Maana mbiu itakapolia, wafu watafufuliwa katika hali ya kutoweza kufa tena, na sisi tutageuzwa.
14 Ila, kabla ya mwisho kufika, hii Habari Njema ya Ufalme wa Mungu itahubiriwa ulimwenguni kote kama ushuhuda kwa mataifa yote.
34 "Muwe macho, mioyo yenu isije ikalemewa na anasa, ulevi na shughuli za maisha haya. La sivyo, Siku ile itawajieni ghafla.
35 Kwa maana itawajia kama mtego, wote wanaoishi duniani pote.
36 Muwe waangalifu basi, na salini daima ili muweze kupata nguvu ya kupita salama katika mambo haya yote yatakayotokea, na kusimama mbele ya Mwana wa Mtu."
15 Hili tunalowaambieni ni fundisho la Bwana; sisi tulio hai, ambao tutakuwa tumebaki, wakati Bwana atakapokuja, hakika hatutawatangulia wale waliokwisha fariki dunia.
16 Maana patatolewa amri, sauti ya malaika mkuu, sauti ya tarumbeta ya Mungu, naye Bwana mwenyewe atashuka kutoka mbinguni. Ndipo wale waliokufa wakiwa wanamwamini Kristo watafufuliwa kwanza.
17 Kisha sisi tulio hai wakati huo tutakusanywa pamoja nao katika mawingu kumlaki Bwana hewani. Na hivyo tutakuwa daima pamoja na Bwana.
18 Basi, farijianeni kwa maneno haya.
29 "Mara baada ya dhiki ya siku hizo, jua litatiwa giza, mwezi hautaangaza, nyota zitaanguka kutoka angani, na nguvu za mbingu zitatikiswa.
30 Kisha, ishara ya Mwana wa Mtu itaonekana angani, na hapo makabila yote duniani yatalalamika; watamwona Mwana wa Mtu akija juu ya mawingu ya angani mwenye nguvu na utukufu mwingi.
31 Naye atawatuma malaika wake wenye tarumbeta la kuvuma sana, nao watawakusanya wateule wake kutoka pande zote nne za dunia, toka mwisho huu wa mbingu hadi mwisho huu.
8 Lakini, wapenzi wangu, msisahau kitu kimoja! Mbele ya Bwana, hakuna tofauti kati ya siku moja na miaka elfu; kwake yote ni mamoja.
9 Bwana hakawii kutimiza yale aliyoahidi kama watu wengine wanavyofikiri kuwa atakawia. Yeye ana saburi kwa ajili yenu, maana hapendi hata mmoja wenu apotee, bali huwavuta wote wapate kutubu.
10 Siku ya Bwana itakuja kama mwizi. Siku hiyo, mbingu zitatoweka kwa kishindo kikuu; vitu vyake vya asili vitateketezwa kwa moto, nayo dunia itatoweka pamoja na kila kitu kilichomo ndani yake.
11 Maadamu kila kitu kitaharibiwa namna hiyo, je, ninyi mnapaswa kuwa watu wa namna gani? Mnapaswa kuishi kitakatifu na kumcha Mungu,
12 mkiingojea Siku ile ya Mungu na kuifanya ije upesi--Siku ambayo mbingu zitateketezwa kwa moto na kuharibiwa, na vitu vyake vya asili vitayeyushwa kwa joto.
13 Lakini sisi, kufuatana na ahadi yake, twangojea mbingu mpya na dunia mpya ambayo imejaa uadilifu.
42 Basi, kesheni, kwa maana hamjui siku atakayokuja Bwana wenu.
43 Lakini kumbukeni jambo hili: kama mwenye nyumba angejua siku mwizi atakapofika, angekesha, wala hangeiacha nyumba yake ivunjwe.
44 Kwa hiyo, nanyi pia muwe tayari, kwa maana Mwana wa Mtu atakuja saa msiyoitazamia."
1 Kisha nikaona mbingu mpya na dunia mpya. Mbingu ile ya kwanza na dunia ile ya kwanza vilikuwa vimetoweka, nayo bahari pia haikuweko tena.
2 Nikaona mji mtakatifu, Yerusalemu mpya, ukishuka kutoka kwa Mungu mbinguni. Ulikuwa umetayarishwa vizuri kama bibi arusi aliyepambwa tayari kukutana na mumewe.
3 Kisha nikasikia sauti kubwa kutoka katika kiti cha enzi ikisema, "Tazama! Mungu amefanya makao yake kati ya watu. Atakaa kati yao, nao watakuwa watu wake, naye atakuwa Mungu wao.
4 Yeye atayafuta machozi yao yote; maana hakutakuwako tena na kifo, wala uchungu, wala kilio, wala maumivu; maana ile hali ya kale imepita!"
1 Kumbuka kwamba, katika siku za mwisho kutakuwa na nyakati za taabu.
2 watu watakuwa na ubinafsi, wenye tamaa ya fedha, wenye majivuno, wenye kujiona, wenye kumtukana Mungu, wasiowatii wazazi wao, wasio na shukrani na waovu;
3 watatokea watu wasio na upendo moyoni, wasio na huruma, wachongezi, walafi na wakali; watachukia chochote kilicho chema;
4 watakuwa wahaini, wakaidi na waliojaa kiburi; watapenda anasa kuliko kumpenda Mungu.
5 Kwa nje wataonekana kama watu wenye kumcha Mungu, lakini wataikana nguvu yake. Jiepushe kabisa na watu wa namna hiyo.
32 "Lakini hakuna mtu ajuaye siku au saa hiyo itakuja lini; wala malaika wa mbinguni, wala Mwana; Baba peke yake ndiye ajuaye.
20 Wafundisheni kushika maagizo yote niliyowapeni. Nami nipo pamoja nanyi siku zote; naam, mpaka mwisho wa nyakati."